mtoto.news

Nairobi, Mombasa, Kisumu: Serikali yafunga shule za kutwa kutokana na maandamano

July 19, 2023

Shule za kutwa zatiwa kufuli kabla ya maandamano ya kuipinga serikali nchini Kenya

Shule za kutwa jijini Nairobi, Mombasa na Kisumu zimefungwa kwanzia Jumatano, Julai 19, 2023, kabla ya uanzishi wa maandamano wa siku tatu mfululizo wa kuipinga serikali ambayo mara nyingi yamekuwa na vurugu.

Katika taarifa ya pamoja ya Jumanne, Julai 18, 2023, Katibu wa Baraza la Mawaziri wa Elimu Ezekiel Machogu na Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki walisema taarifa za kijasusi za usalama zilionyesha kuwa wahalifu wanapanga kusababisha ugaidi na ghasia kwa umma wakati wa maandamano ambayo yamepangwa kufanyika Jumatano hadi Ijumaa.

Taarifa hiyo ilisema kwamba, wahalifu hao wananuia kuhusika katika makabiliano yenye silaha na mashirika ya usalama karibu na shule fulani Nairobi, Mombasa na Kisumu.

“Kama hatua ya tahadhari ya kuhakikisha usalama wa watoto wa shule, imeamuliwa kuwa shule za msingi na upili za kutwa katika miji ya Nairobi, Mombasa na Kisumu zitasalia kufungwa kesho,” taarifa ya Machogu na Kindiki ilisema.

Hata hivyo, walinena kwamba, tarehe za ufunguzi zitatangazwa baada ya kutathminiwa kwa hali ya usalama nchini. “Wizara ya Elimu itatangaza kuanza tena kwa masomo katika shule zilizotajwa hapo juu baada ya kutathmini hali ya usalama katika mwendo wa kesho.”

Kauli hiyo ya serikali imekuja wakati viongozi wa Azimio wakiapa kuendelea na maandamano waliyopanga nchi nzima kupinga gharama kubwa ya maisha pamoja na mambo mengine.

Walimu wameonya kuwa huenda wanafunzi wakapoteza hadi masaa Ishirini ya masomo kutokana na maandamano ya siku tatu yaliyopangwa dhidi ya serikali. Wanafunzi wa shule za msingi watapoteza masaa 14, huku wa shule za sekondari wakipoteza takriban masaa Ishirini.

Vilevile, siku ya Jumanne wadau wa elimu walikashifu athari za maandamano hayo kuhusu elimu. Mwenyekiti wa Chama cha Wakuu wa Shule za Msingi nchini Kenya Johnson Nzioka alionya kuhusu ‘usumbufu mkubwa’ kwa sababu ya maandamano hayo. Alisema kwamba, wanafunzi wengi ambayo ni sawa na asilimia 70 wanasoma shule za msingi na sekondari za kutwa, na wao ndio wanaoathirika zaidi.

“Kuongezeka kwa mvutano kutoka kwa maandamano ya awali kumesababisha baadhi ya wanafunzi na walimu kutoroka shule, na hii inapunguza kasi ya ufunzaji na ujifunzaji, na hatimaye kusababisha kuchelewa kuwasilishwa kwa silabasi,” Nzioka aliambia The Standard.

Wadau wengine walionya uharibifu huo unaweza kudumu kwa muda mrefu. Na pasipo na elimu, basi watoto na vijana wanaweza kukabiliwa na unyanyasaji na ukatili.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *